HALMASHAURI ZINAZODAIWA FEDHA ZA MRADI WA KUPANGA, KUPIMA NA KULIKISHA ARDHI ZABANWA
Posted On: 17th March, 2021
Na Eliafile Solla
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imezitaka Halmashauri zote
nchini ambazo zilikopeshwa fedha na Wizara ya Ardhi kwa ajili ya mradi wa
Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi kurejesha fedha hizo kabla ya tarehe 25
Machi, 2021 ili fedha hizo ziweze kukopeshwa kwa Halmashauri nyingine ambazo
bado hazijapanga, wala kupima maeneo yao.
Agizo
hilo limetolewa Mkoani Iringa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Utalii Mhe. Aloyce A. Kwezi wakati kamati hiyo ilipotembelea na
kukagua mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo ambao
umetekelezwa na Manipsaa ya Iringa kwa kutumia fedha hizo za mkopo walizopewa
na Wizara ya Ardhi.
‘‘Kimsingi
kazi ya upangaji miji ni jukumu la kila Halmashauri na siyo Wizara hivyo ni
lazima mtambue kwamba Wizara iliwasaidia katika kutekeleza majukumu yenu ya
msingi kuwakopesha fedha na ndiyo maana mkopo huo haukuwa na riba ili mkapange,
mpime na mmlikishe wananchi ardhi kwenye Halmashauri zenu’’ alisema Kwezi.
Kwa
upande wake Mhe. Angelina Mabula Naibu
Waziri Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliishukuru Kamati hiyo
ya Bunge na kusema nia ya Serikali kupitia Wizara ni kuona kila kipande cha
ardhi nchini kinapimwa na hivyo Wizara iliamua kuziwezesha Halmashauri zenye
dhamana ya upangaji miji katika maeneo yao kwa kuzikopesha kiasi cha fedha ili
zitumike katika utekelezaji wa kazi hizo za upangaji,upimaji na umilikishaji
ardhi na kisha kuzirejesha.
Mabula
aliongeza kwamba, Wizara kwa kuanzia ilitoa mikopo ambayo haina riba kwa
Halmashauri 24 nchini kwa lengo la kupunguza migogoro kwa kuwapimia wananchi
maeneo yao na kuzisaidia Halmashauri kuongeza kipato ambapo walikuwa na uwezo
wa kupima maeneo na kuyauza ila hadi sasa ni Halmashauri saba tuu zimerejesha
fedha hizo za Wizara kitu kinachokwamisha mradi kutekelezwa na Halmashauri
nyingine kwani mradi ulitakiwa kuwa endelevu.
Mradi
wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi wa Igumbilo Manispaa ya Iringa, ulianza
kutekelezwa kuanzia 2019/2020 kwa fedha ya mkopo kutoka Wizara ya Ardhi, ambapo
jumla ya viwanja 375 vilipimwa na kati ya hivyo viwanja 253 vilikuwa na sifa ya
kuuzwa na 122 havikuwa na sifa ya kkuza kutokana na sababu mbalimbali.