Habari
WIZARA YA ARDHI KUTOA ELIMU NYEPESI KUHUSU UMILIKI ARDHI
- 25 Sep, 2023
Na Munir Shemweta, WANMM BAGAMOYO
Waziri wa ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa amesema wizara yake iko mbioni kutoa elimu nyepesi kwa wananchi kuhusu hatua mbalimbali za umiliki ardhi na jinsi ardhi inavyoweza kuhamishwa kutoka mmiliki moja kwenda kwa mwingine.
Amesema hayo tarehe 23 Septemba 2023 wakati wa akizindua Clinic ya Ardhi kwa wilaya ya Bagamoyo inayoendelea eneo la Mapinga mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa Silaa, pamoja na wizara yake kuwa na jukumu la kuisimamia ardhi ipo haja kutoa elimu nyepesi kwa watanzania kwenye eneo la ardhi kuanzia inapotwaliwa, kupangwa, kupimwa na kumilikishwa hususan inapohama kutoka mmiliki mmoja kwenda mwingine.
"Tukitoa hiyo elimu inaweza kusaidia maana hapa kuna watu wamenunua eneo kwa mwenyekiti wa mtaa wakiamini wana eneo lakini sheria ya ardhi haielekezi kupata eneo kwa mwenyekiti wa mtaa" alisema
Akifafanua zaidi, Waziri wa Ardhi amesema anayenunua ardhi kwa mtu anao wajibu wa kujua ama kufahamu aliyemuuzia ameipataje ardhi ambapo amesema maeneo mengine na mauzo hayo yanashuhudiwa na viongozi wakiwemo wenyeviti wa vitongoji.
Hata hivyo, ameweka wazi kuwa, pamoja na wamiliki wa ardhi wa kulinda maeneo yao wanayomiliki lakini wizara yake haitaacha maeneo kama Mapinga Bagamoyo kuwa kichaka cha mtu yeyote mwenye uwezo kufanya anachotaka anafanya.
''Niweke wazi mimi katika uongozi wangu wizara ya ardhi nitakachofanya ni kuhakikisha nasimamia haki na siku zote haki haina rangi jinsia, haina hali ya mtu na haki ni haki''. alisema
Amewataka wananchi kuheshimu sheria zinazotungwa na Bunge sambamba na kujifunza kusimamia haki zao.
''Wapo baadhi ya viongozi wa wanaotumia mamlaka yao ya kutambua maeneo na kuwekea ushahidi lakini sheria ya ardhi haiwataji kama wanapaswa kufanya miamala ya ardhi''. Alisema Waziri Silaa.
''Tunataka na wenzaTu katika majiji makubwa kama Mwanza, Dodoma Arusha, Dar, Mbeya na Pwani ambayo kiasi kikubwa inaungana na Dar es Salaam ifike wakati tufanye kazi za ardhi kwa mujibu wa sheria'' alisema
Awali Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Halima Okashi alieleza kuwa, Clinic ya Ardhi waliyoianzisaha itakuwa na jukumu la kusikiliza kero za wananchi katika masuala ya mbalimbali ya ardhi huku akibainisha kuwa, itaendelea katika kata zote za wilaya ya Bagamoyo.
Uzinduzi wa Clinic ya Ardhi katika wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani unafuatia uzinduzi wa Clinic kama hizo kwenye wilaya ya Kigamboni na Temeke ambapo lengu kubwa ni kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za sekta ya ardhi.