Habari
MRADI WA UBORESHAJI USALAMA WA MILKI ZA ARDHI UTATUE KERO ZA ARDHI- WAZIRI SILAA
- 27 Sep, 2023
Na Magreth Lyimo, WANMM
Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umetakiwa kuangalia namna bora ya kufikia maeneo yenye migogoro ya ardhi ili kuongeza idadi ya wananchi wenye nyaraka za kumiliki ardhi.
Kwa kufanya hivyo kutapelekea kupunguza migogoro ya ardhi iliyopo na kuongeza usalama wa milki za ardhi kwa Watanzania ambalo ni lengo kuu la mradi huo wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi.
Hayo yamebainishwa tarehe 26 Septemba 2023 jijini Dodoma na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa wakati akipokea taarifa ya Mradi kutoka kwa Mratibu wa mradi huo Bw. Joseph Shewiyo.
‘‘Tulikuwa na ziara ya Mhe. Rais katika mkoa wa Mtwara, Lindi na maeneo mengine ya jirani na suala la migogoro ya matumizi ya ardhi lilijitokeza hivyo ni vyema mradi uangalie namna ya kutatua changamoto hizo kwa Watanzania’’ alisema Silaa.
Mratibu wa Mradi Bw. Shewiyo alimueleza Waziri Silaa kuwa, mpaka sasa katika kipindi cha awamu ya kwanza, mradi unaendelea kutekelezwa kwenye halmashauri mbalimbali nchini na kuzitaja kuwa ni Dodoma Jiji, halmashauri ya wilaya ya Chalinze, Mufindi, Chamwino, Longido, Maswa, Tanganyika, Songwe, Mbinga pamoja na Manispaa za Kigoma Ujiji na Kahama.
‘‘Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam, mradi umeanza kutekeleza program ya ukwamuaji urasimishaji katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Halmashauri zilizobakia baada ya hatua ya kuutambulisha mradi kazi ya ukwamuaji urasimishaji itaendelea kwa mujibu wa ratiba’’ alifafanua Shewiyo.
Akieleza zaidi kuhusiana na mradi huo, alisema mbali na utoaji Hati takribani milioni mbili na laki tano, mradi utafanya maandalizi ya ramani za msingi, uboreshaji mfumo wa ILMIS, mifumo ya uthamini sambamba na ujenzi wa ofisi za ardhi katika mikoa 25 ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Shewiyo, kazi nyingine zitakazofanyika kupitia mradi wa LTIP ni ukarabati ofisi za ardhi kwenye halmashauri 41, uboreshaji ofisi za Mabaraza ya Ardhi katika halmashauri 41, ukarabati wa masijala za ardhi za vijiji 250, kuwajengea uwezo watumishi pamoja na uratibu wa masuala ya kijamii na mazingira.
Ikumbukwe kuwa mradi wa uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi ni mradi ulio chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na utekelezaji wake umeanza mwaka 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2026.
Lengo la mradi wa LTIP ni kuimarisha usalama wa milki za ardhi kwa kuongeza idadi ya watanzania wenye nyaraka za kumiliki ardhi kwa kuzingatia jinsia, kuimarisha miundo mbinu ya msingi ya usimamizi wa ardhi, kujenga uwezo kwa watendaji na mamlaka za usimamizi wa ardhi pamoja na kutoa elimu ya masuala ya ardhi kwa wananchi.