WAZIRI WA MAENDELEO YA MIJI NA VIJIJI WA NAMIBIA AFIKA NCHINI KUJIFUNZA UTAWALA WA ARDHI
Posted On: 23rd August, 2016
Waziri wa Maendeleo ya Miji
na Vijiji wa Namibia; Sophia Shaningwa amefika nchini na ujumbe wa Wataalamu wake kwa ajili ya
kujifunza taratibu za Utawala wa Ardhi wa Tanzania.
Akizungumza na Naibu Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula (Mb), ofisini kwake; Waziri
huyo ameeleza kuwa Bunge nchini Namibia limewaelekeza kufika Tanzania kujifunza
taratibu zinazofanywa katika eneo la Utawala wa Ardhi, baada ya Bunge hilo
kuona mfano mzuri wa nchi ya Tanzania kati ya nchi nyingine za Afrika
walizofanyia tathimini katika eneo hilo.
Aidha, Waziri huyo ameeleza
kuwa amenufaika sana kwa kujifunza mengi mazuri, na amependa zaidi utaratibu mzuri uliopo katika
eneo la uwekezaji wa ardhi, na kusema
kuwa atafanyia kazi yale aliyojifunza.
Kwa upande wake Mhe. Mabula
amesema amefarijika kuona kuwa jopo hilo limeona mazuri yaliyomo ndani ya
Utawala wa Ardhi nchini Tanzania. Aliendelea
kusema; “ Sekta ya Ardhi bado ina changamoto nyingi, hasa ile ya
Migogoro iliyopo kati ya Wakulima na Wafugaji, hatahivyo Wizara inajitahidi
kuendelea kukabiliana na changamoto hiyo”.