SERIKALI iko mbioni kutoa
hatimiliki zaidi ya 25,000 kwa wakazi wa kata za Kimara na Saranga zilizopo
jijini Dar es Salaam ikiwa ni hatua ya kurasimisha makazi holela.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es
Salaam na Mratibu wa Mradi wa urasimishaji wa makazi holela Kata za Kimara na
Saranga, Bi Grace Masatu wakati wa zoezi la ukaguzi wa maeneo ya mradi.
“Zoezi za la upimaji linaenda
sanjari na utambuzi wa mipaka,ujazaji wa madodoso, uchoraji wa ramani za
upimaji na mipangomiji,”alisema Masatu.
Viwanja zaidi ya 25,000
vinatarajiwa kupimwa katika kata za Kimara na Saranga ambapo hadi leo ramani za
upimaji 14 na ramani sita (6) za mipangomiji zenye jumla ya viwanja1028 ziko
tayari na zimeshawasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
ajli ya kupitishwa, alisema Masatu.
Aidha, Masatu amesema kuwa
malengo ya mradi huo ni kuongeza thamani ya makazi kwa kutoa hatimiliki na
kutambua mipaka ya wakazi wa maeneo husika.
Kwa upande wake, Afisa Mipango
miji Mkuu, Bi Anna Macha, alisema kuwa hadi sasa maeneo yaliyopimwa katika kata
ya Kimara ni mtaa wa Kilungule A wote pamoja na viwanja 724 vya mtaa wa
Kilungule B, ambavyo vimechukuliwa mahesabu ya upimaji kwa ajili kuandaa
ramani.
Ameongeza kuwa umetengenezwa
mfumo maalum ambao unachukua taarifa za madodoso zinazojazwa wakati wa utambuzi
wa mipaka ya wamiliki wa maeneo husika. Mfumo huo utaunganishwa na mfumo wa
Kamishna wa Ardhi (MOLIS) utakaorahisisha kufahamu idadi ya viwanja
vilivyopimwa na kumilikishwa.
Naye Mjumbe wa Mtaa wa Kilungule
B, Bwana Claud Misri Silayo ameonyesha
kuridhishwa na zoezi zima la utambuzi na upimaji wa maeneo.
“ Nimefurahishwa na zoezi la
upimaji kwani nitamiliki ardhi kisheria, kihalali na nitafaidika na ardhi
ninayomiliki kwa sababu mwisho wa zoezi hili nitapata hatimiliki ambayo
itaniwezesha kupata mikopo kwenye taasisi za fedha,”alisema Silayo.
Urasimishaji ni mwendelezo wa
utambuzi wa makazi holela katika jiji la Dar es Salaam unaotekelezwa chini ya
Sheria ya Ardhi Na. 4 pamoja na Sheria ya Mipangomiji.