MGOGORO WA ARDHI WA KIJIJI CHA MABWEGERE NA VIJIJI JIRANI WILANI KILOSA, MKOANI MOROGORO KUCHUNGUZWA KISHERIA.
Posted On: 19th July, 2016
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William
Lukuvi, amemteua, Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania Kitengo cha Biashara Bwn. Jacob Mwambegele kuwa mchunguzi wa
mgogoro sugu wa Ardhi katika Vijiji vya Mabwegele, Kambaya na vijiji jirani vya
Mfulu, Mbigiri, Dumila, Mambwega na Matongolo vyote vya Wilayani Kilosa mkoani Morogoro
Akizungumza wakati akimkabidhi Jaji Mwambegele taarifa ya kamati
ya Usuluhishi ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mhe. Lukuvi alisema uamuzi
huo ni wa kisheria na ameuchukua baada ya hatua ya awali ya usuluhishi
kutofikia malengo
Kabla ya uteuzi wa Jaji Jacob, msuluhishi wa mgogoro huo
aliyeteuliwa alikuwa Bwn. Stephen Mashishanga ambae aliifanya kazi hiyo na
kushindwa kuikamilisha baada ya upande mmoja kususia kikao cha usuluhishi. Baada
ya hatua hiyo kushindikana, Mhe. Lukuvi ameamua kuteua mchunguzi kwa mujibu wa
Sheria ya Ardhi kifungu namba 18 sura ya 113 na kifungu cha 7 (2) (a) sura ya
114 cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji.
Waziri Lukuvi alisema, uteuzi wa Jaji Mwambegele ni sambamba
na kamati ya watu 8 ambao watafanya kazi hiyo ya uchunguzi kwa muda wa siku 60
ili kubaini chanzo cha mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 27 na
kusababisha madhara mbalimbali kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro.
Katika uchunguzi huo, mambo yatakayoangaliwa zaidi ni pamoja
na; uhalali wa kisheria wa uanzishwaji
wa kijiji cha Mabwegele, jinsi ardhi ya kijiji hicho ilivyopimwa kabla ya
kuanzishwa kwa kijiji , kuchuguza iwapo ardhi ya kijiji hicho inatosheleza
mahitaji ya wanakijiji wote wakiwepo wakulima na wafugaji, kufahamu kwa nini
baadhi ya viongozi wa kijiji walisusia kamati ya usuluhishi ya awali.