VIJIJI 46 KUENDELEA NA SHUGHULI ZA KIBINADAMU ENEO KINGA SIMIYU
Posted On: 18th October, 2022
Na Munir Shemweta, WANMM
SIMIYU
Serikali imeruhusu vijiji 46 katika mkoa wa Simiyu vilivyokuwa
katika mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya hifadhi kuendelea na
shughuli za kibinadamu ambazo hazitaathiri shughuli za uhifadhi wa wanyama pori
na ndani ya eneo kinga la mita 500.
Aidha, vijiji viwili kati ya 48 vya mkoa wa Simiyu vilivyokuwa
katika mgogoro wa aina hiyo vinafanyiwa tathmini ili kumega eneo ndani ya
hifadhi ya Jumuiya ya Jamii (WMA).
Vijiji 46 vilivyoruhusiwa ni vile vilinavyoendesha shughuli za
kibinadamu kwenye eneo kinga la mita 500 linalotenganisha vijiji hivyo na hifadhi
ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba la Maswa pamoja na pori la akiba la
Kijereshi.
Hayo yamebainishwa tarehe 17 Oktoba 2022 mkoani Simiyu na Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline katika kikao baina ya
Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta na viongozi wa mkoa na wilaya
kupeleka mrejesho wa Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya
matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
pamoja na uamuzi huo wa serikali uliotolewa mkoa utakuwa na jukumu la kusimamia
utekelezaji wa maamuzi hayo kwa kushirikiana na taasisi na mamlaka zote
zilizopo ndani ya mkoa.
"Kamati ya wataalamu inayojumuisha wataalamu kutoka ngazi
ya taifa, mkoa, wilaya na taasisi zetu za uhifadhi ilianza kazi za tathmini
katika vijiji husika mwezi septemba 2022" alisema Dkt Mabula.
Dkt Mabula aliongeza kuwa, tathmini iliyofanyika inahusisha
kufanya vikao na viongozi wa serikali za vijiji na kuembelea eneo la kinga la
mita mia tano kubaini matumizi yaliyopo sasa.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Khamis Hamza
Chillo akizungumza katika kikao hicho alisisitiza suala la elimu ya sheria ya
utunzaji mazingira na vyanzo vya maji ili kuepuka uharibifu unaoweza kufanywa
na binadamu.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde alieleza nia ya
Wizara yake kutungwa kwa sheria ya kilimo ili kulinda ardhi ya kilimo kwa lengo
la kuboresha sekta hiyo nchini.
Baadhi ya Mapendekezo ya kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta
kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni pamoja na kubakisha
vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi
yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa wananchi sambamba na kuhakiki na kurekebisha
mipaka kati ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.
Pia yapo mapendekezo ya kumega baadhi ya hifadhi na kugawia
wafugaji na wakulima, kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya
ardhi, kupitia upya sheria ya vyanzo vya maji inayozungumzia mita 60 na kufutwa
kwa mashamba yasiyoendelezwa.