NEWALA MJI YAANZA KUTEKELEZA MAAGIZO YA WAZIRI WA ARDHI
Posted On: 18th October, 2022
WANMM, MTWARA
Halmashauri ya Mji wa Newala mkoa wa Mtwara imeanza kutekeleza
maagizo ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline
Mabula ya kuzitaka halmashauri zote nchini kuhakikisha zinapima na kumilikishwa
maeneo yake yakiwemo ya shule, zahanani na vituo vya mabasi ili kuepuka
migogoro ya ardhi.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Newala Shamim Daudi Mwariko
alikabidhiwa jumla ya hati saba na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara
Rehema Mwinuka ambapo hati tano kati ya alizokabidhiwà ni za shule za
msingi na hati mbili ni za zahanati.
Shule za msingi zilizopata hatimiliki za ardhi ni Mtangalanga,
Kiduni, Butiama, Mcholi II na Mkoma I huku upande wa zahanati zikiwa ni Mkoma I
na ile ya Makondeko.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi hati hizo mkoani Mtwara jana
Kamishna wa Ardhi mkoa wa Mtwara Rehema Mwinuka aliipongeza halmashauri ya Mji
wa Newala kwa uamuzi wa kupimiwa maeneo yake na kuzitaka halmashauri
nyingine katika mkoa huo kuiga mfano wa halmashauri hiyo kwa kupima na kumilikishwa
maeneo yake ili kuepuka uvamizi katika maeneo hayo.
"Nichukue fursa hii kuwapongeza halmashauri ya Mji wa
Newala kwa uamuzi wenu wa kupima maeneo yenu, hii itasaidia sana kupunguza
migogoro ya ardhi inayotokana na uvamizi na niombe hakmashauri nyingine ziige
mfano wenu" alisema Rehema.
Mbali na kukabidhi hati kwa halmahauri ya Mji wa Newala kamishna
wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mtwara aliwaongoza watumishi wa mkoa wake kutoa hati
kwa wamiliki wa ardhi waliokamikisha taratibu za kupatiwa hati sambamba na
kusikiliza na kutatua changamoto za sekta ya ardhi katila kituo jumuishi.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha
utaratibu wa ofisi zake za ardhi katika mikoa kuwa na vituo jumuishi vya
kusikiliza na kutatua changamoto za ardhi pamoja na kutoa hatimiliki za ardhi
ikiwa ni juhudi za kusogeza huduma karibu na wananchi.