MAWAZIRI WIZARA ZA KISEKTA WATEMBELEA MAENEO YA HIFADHI NA CHANZO CHA MAJI YALIYOVAMIWA KATAVI
Posted On: 18th October, 2022
Na Munir Shemweta, WANMM KATAVI
Kamati ya Mawaziri wa
Wizara za Kisekta imetembelea maeneo ya hfadhi na chanzo cha maji katika mkoa
wa Katavi kujionea hali ya uvamizi wa maeneo hayo na kuelekeza wananchi waliovamia
maeneo hayo kutofanya maendelezo mpaka hapo timu ya wataalamu itakapokamilisha
kazi yake kuhusiana na mgogoro wa matumizi ya ardhi kwenye maeneo hayo.
Kamati hiyo
inayohusisha Wizara nane za kisekta Oktoba 12, 2022 ilitembelea eneo la hifadhi la mito miwili
lilipo kitongoji cha Kasekese wilayani Tanganyika pamoja na chanzo cha maji cha
Milala kilichopo kata ya Misunkumilo manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Kiongozi wa Kamati ya
Mawaziri wa Kisekta katika ziara hiyo Mhe. Mashimba Ndaki aliwaeleza wananchi
wa Kisekese kuwa, uamuzi wa mwisho kama eneo hilo liendelee kuwa hiadhi au
maeneo ya kuishi watu itajulikana baada ya kupata majibu kutoka kwa wataalamu.
''Ndugu wananchi naomba
mnielwe eneo hili mnalolikalia halijaeleweka kama ni makazi yenu na vizuri
tuelewe ingawa ukweli wenyewe mgumu lakini ni vizuri kuelewa kwa sababu lina
sura mbili ni eneo la hifadhi au kupita wanyama lakini ninyi mpo mmekaa''
alisema Ndaki.
Aliwataka wananchi hao kuwa
wavumilivu wakati wataalamu wanafanyia kazi suala hilo na kamati yake ikishapa
majibu kuhusiana na suala hilo basi uamuzi kamili wataelezwa kati ya mambo mawili
ambayo ni ama eneo hilo ni hifadhi au eneo la kupita wanyama.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete aliwaeleza
wananchi wa Kasekese katika mkutano wa hadhara kuwa, kwa mujibu wa sheria za ugawaji
ardhi hakuna mahali popote panaposema kuwa kiongozi anaweza kugawa ardhi kwa
wananchi.
''Sheria hizi zote
mbili nilizozitaja hakuna hata sheria moja iliyompa mamlaka mkuu wa wilaya au
mkuu wa mkoa kugawa ardhi na ndiyo maana nimestuka sana niliposikia kuwa kuna
mkuu wa wilaya amewachukua watu na kwenda kuwagawia ardhi, huyo mkuu wa wilaya
amewaingiza chaka'' alisema Ridhiwani.
Akigeukia suala la
chanzo cha maji cha Milala kilichopo Manispaa ya Mpanda, Waziri Ndaki
aliwaambia wananchi wanaoishi eneo hilo kuwa, taarifa za awali zinaonesha kuwa wananchi
hao wamevamia chanzo hicho na wanatakiwa kuondoka. Hata hivyo, alibainisha kuwa,
uamuzi wa mwisho wa aidha kubaki ama kuondoka eneo hilo utaamuliwa pale Kamati
yake itakapopata ushauri kutoka serikali ya mkoa wa Rukwa.
Kamati ya Mawaziri nane
wa Wizara za Kisekta iliyoanza kazi kwenye mkoa wa Rukwa imemaliza ziara yake mkoani
Katavi na inaendelea na ziara hiyo katika mkoa wa Kigoma na baadaye Kagera.