KAMATI YA MAWAZIRI WIZARA ZA KISEKTA YAANZA ZIARA MIKOA 14 KUTATUA MIGOGORO YA MATUMIZI YA ARDHI
Posted On: 12th October, 2022
Na Munir Shemweta, WANMM
RUKWA
Mawaziri wa Wizara za Kisekta wameanza ziara ya utatuzi wa
migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Ziara ya Mawaziri hao imeanza leo tarehe 11 Oktoba 2022 katika
mkoa wa Rukwa na itaendelea mkoa wa Katavi tarehe 12 Oktoba 2022 kabla ya
kuelekea Kigoma Oktoba 13, 2022.
Katika mikoa hiyo mitatu ya mwanzo, Kamati ya Mawaziri wa Wizara
za Kisekta itaoongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt Mashimba Ndaki.
Mikoa mingine itakayotembelewa na Kamati hiyo itakayohitmisha
ziara yake Oktoba 28, 2022 mkoani Dar es Salaam ni pamoja na Kagera, Mwanza,
Simiyu, Shinyanga, Njombe, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Wakati wa ziara yake, Kamati itakutana na Sekreterieti za mikoa
na wilaya na kutoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na
utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 pamoja na
kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro.
Baadhi ya Mapendekezo ya kamati kuhusiana na utatuzi wa migogoro
ya matumizi ya ardhi ni kubakisha vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya
hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa
wananchi na kuhakiki pamoja na kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu,
wanyama na makazi.
Pia yapo mapendekezo ya kumega baadhi ya hifadhi na kugawia
wafugaji na wakulima, kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya
ardhi, kupitia upya sheria ya vyanzo vya maji inayozungumzia mita 60 na kufutwa
kwa mashamba yasiyoendelezwa.
Tayari timu za wataalamu kutoka wizara za kisekta ziko uwandani
katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo kuhakikisha Kamati ya Mawaziri inafanya
kazi yake kwa ufanisi
Mawaziri wanaoshiriki ziara hiyo mbali na Mhe Dkt Mashimba Ndaki
ni Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa Joseph Silinde, Naibu Waziri Maliasili na Utalii
Mary Masanja, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Khamis Hamza
Chillo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani
Kikwete.