KAMATI YA PAMOJA WATAALAM WA MIPAKA TANZANIA NA KENYA YAKAGUA MPAKA
Posted On: 13th April, 2022
Na Munir Shemweta, WANMM SERENGETI
Timu
ya Wataalamu wa Mipaka kati ya Tanzania na Kenya imetembelea na
kujionea kazi ya uimarishaji mipaka wa Kimataifa wa nchi hizo
iliyofanywa kwa lengo la kukagua na kushauri namna bora ya kuendelea na
kazi zinazofuta.
Ukaguzi
wa mipaka hiyo ulifanyika tarehe 12 April 2022 na ni sehemu ya kikao
cha pamoja cha Wataalam wa Mipaka wa nchi hizo kilichoanza juzi kwa
ajili ya kupokea mawasilisho ya kazi iliyofanyika sambamba na kutoa
muongozo wa namna bora ya kutekeleza kazi iliyobaki.
Wataalam
hao wakioongozwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansoor pamoja na Juster Nkoroi
Mtendaji Mkuu Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa nchini Kenya (KIBO)
walitembelea mpaka wa Tanzania na Kenya eneo la Kirongwe wilayani Rorya
kwa upande wa Tanzania na Muhuru Bay katika Kaunti ya Migori nchini
Kenya pamoja na ule mpaka wa nchi hizo eneo la Serengeti/Masai Mara ili
kukagua kazi ya uwandani.
Timu
ya wataalamu wa mipaka kutoka nchi za Tanzania na Kenya tayari
imekamilisha uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo kipande cha
Kilomita 83 kutoka hifadhi ya Serengeti/ Masai Mara hadi Ziwa Natron na
awamu ya pili ya kipande cha kilomita 110 uimarishaji wake utaendelea
baada ya kukamilika kuandaliwa mpango kazi.
Wakati
wa ufunguzi wa kikao cha pamoja cha Wataalam wa Mipaka wan chi hizo
mbili, Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mangwela kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa wa Mara aliwaambia washiriki kuwa, uimarishaji mipaka
ulenge kuimarisha mahusiano pia pamoja na kujadili changamoto za maeneo
ya mipakani.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Balozi Joseph
Vungo alishauri wataalamu wanaoshiriki kikao hicho kuhakikisha
wanajadili na kuzitolea maamuzi changamoto kwa amani hasa wakizingatia
nchi ya Tanzania na Kenya zimekuwa na mahusiano mazuri.
Mpaka
wa Tanzania na Kenya eneo la nchi kavu una ukubwa wa Kilomita 758 na
uimarishaji wake utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali zilizokuwa
zikijotokeza kutoka kwa wananchi wanaofanya shughuli maeneo ya mipakani
katika nchi hizo.