WENYEVITI MABARAZA YA ARDHI WATAKIWA KUEPUKA MAZUIO YASIYO NA TIJA
Posted On: 22nd March, 2022
Na Munir Shemweta, WANMM SENGEREMA
Serikali
imewataka Wenyeviti wa Mbaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kujiepusha
na tabia ya uwekaji mazuio yasiyo na tija dhidi ya uuzaji wa nyumba za
wadaiwa wa benki.
Akizungumza
wakati wa kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ya Sengerema
tarehe 21 Machi 2022 jijini Mwanza, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, baadhi ya mazuio huwekwa na kisha
shauri hupangiwa tarehe ya mbali bila sababu ya msingi.
‘’Jambo
hili halikubaliki hata kidogo kwani linarudisha nyuma shughuli za
kimaendeleo na kukuza uchumi wan chi yetu ‘’ alisema Dkt Mabula.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kutoa kipaumbele katika
kuyawezesha Mabaraza ya Ardhi kufanya kazi vizuri na tayari imeanza
kufanya maboresho ya muundo wa wizara utakaowezesha kila mkoa kuwa na
Msajjili Msaidizi wa Mabaraza kwa ajili ya usimamizi wa karibu wa
utendaji kazi wa Mabaraza.
Vile
vile, kwa mujibu wa Dkt Mabula Serikali imeendelea kuchukua hatua
mbalimbali ambapo katika kuboresha mazingira ya utendaji kazi imefanya
mabadiliko ya sheria ili kuwawezesha Wenyeviti wa Mabaraza kuwa na ajira
za kudumu.
Aliwakumbusha
watumishi wote wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini kutimiza
majukumu yao kwa weledi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na
miongozi iliyopo na ile itakayokuwa ikitolewa ili kuboresha utoaji
huduma ya utatuzi wa migogoro itokanayo na matumizi ya ardhi.
Pia
Waziri wa Ardhi Dkt Mabula aliwataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi
kuwafuata wananchi kwa kutembelea mabaraza mapya ili kusikiliza mashauri
kwenye wilaya husika wakati Wizara ikiendelea kukamilisha taratibu za
ajira za wenyeviti wa mabaraza hayo.
Kwa
upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya Stella
Tullo alisema, ofisi yake imejipanga na kuhakikisha migogoro ya ardhi
inapofika kwenye Mabaraza inasikilizwa kwa haki na kwa haraka na
kusisitiza kuwa, hawatopenda kuchelewesha mashauri bila sababu za
msingi.
‘’Sisi
tunataka shauri linapofika kwenye Baraza liweze kuanza kusikilizwa
mapema baada ya taratibu za awali za kisheria kukamilika ili tuweze
kukamilisha kwa wakati’’ alisema Stella
Uzinduzi
wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Sengerema uliwakilisha pia uzinduzi wa
mabaraza mengine mapya katika wilaya za Nachingwea, Ruangwa, Liwale,
Kilwa, Serengeti, Kongwa , Kishapu na Mlele.