TANZANIA NA KENYA ZAKAMILISHA ZOEZI LA UWEKAJI VIGINGI VYA MIPAKA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI
Posted On: 21st March, 2022
Na Antony Ishengoma, WANMM
Serikali ya Tanzania na Kenya zimekamilisha zoezi la uwekaji vigingi
katika mpaka unaoigawa Tanzania na Nchi jirani ya Kenya katika mbuga ya
Serengeti na hivyo kufanikiwa kumaliza mgogoro wa mpaka uliokuwepo
hususani katika sekta ya utalii kati ya nchi zote mbili.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete
alisema hayo jana wakati yeye na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili
na Utalii walipofika katika Mbuga ya Serengeti kujionea utekelezaji huo
unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi.
Naibu Waziri Kikwete alisema zoezi la uwekaji vigingi katika mpaka huo
wenye zaidi ya Km 83 utaiwezesha Serikali kupata mapato na sifa ambayo
mbuga ya Serengeti iko nayo, akiongeza kuwa vingi hivyo vimewekwa karibu
zaidi tofauti na awali ambapo vingingi hivyo viliwekwa kwa umbali
mkubwa na kuwa ngumu zaidi kuvitambua.
‘’Katika kipindi cha mwaka mmoja Serikali ya Rais Samia na ile ya Kenya
ziliweza kuingia katika makubaliano ambayo matokeo yake yamewezesha
kutatua mgogoro uliokuwepo katika mpaka ndani ya mbuga ya Serengeti na
kuleta heshima kubwa kwa nchi zote mbili.
Naibu Waziri huyo alitumia fursa hiyo kupongeza mafanikio ya Serikali
kwa kipindi cha mwaka mmoja nakubainisha kuwa zoezi kama hilo pia
litaendelea kati ya mipaka ya nchi nyingine jilani ikiwemo Uganda,
Malawi na Kongo hasa katika mipaka iliyo ndani ya maji.
Naye Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Utalii Ally Makoa amewaagiza watendaji wa Wizara kuhakikisha
wanatekeleza zoezi hilo na kuharakisha uweka vingingi katika mpaka,
ili kuondokana na adha iliyopo katika utambuzi wa mipaka inayoigawa
Tanzania na nchi jirani.
“kazi hii iliyofanyika ni kazi nzuri sana na tunatamani sasa maeneo yetu
yote yaliyohifadhiwa yawe na vigingi vya mipaka vinayoonekana kwa
malengo yaleyale tuliyoyafanya hapa katika maeneo yote ya nje na ndani
ya nchi kuwe na vigingi vivyoonekana ili pasiwe na uvamizi”. Makoa
aliongeza
Wizara ya ardhi itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na yale ya
kibajeti na kutoa kipaumbele katika utatuzi wa migogoro baina ya Nchi
jirani kwa kuweka vingingi katika mipaka ambavyo awali viliwekwa na
wakoloni katika umbali mrefu na kusababisha sintofahamu katika baadhi ya
maeneo.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imehitimisha
ziara ya kikazi kwa kutembelea program mbalimbali zinazotekelezwa na
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada kufuatilia
utekelezaji wa miradi hiyo katika Mkoa wa Singida, Mwanza na Mara.