Aliyekuwa
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
amemkabidhi Ofisi aliyekuwa Naibu wake Dkt Angeline Mabula ambaye sasa
ni Waziri wa Wizara hiyo.
Makabidhiano
ya ofisi yamefanyika leo tarehe 17 Februari 2022 kwenye ofisi za Wizara
hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma.
Akizungumza
wakati wa makabidhiano hayo, Lukuvi alisema ana furaha kubwa kumkabidhi
ofisi mtu anayeijua Wizara na aliyekuwa akifanya kazi naye.
‘’
Dkt Angela anayajua mengi kwenye wizara, tumeshirikiana katika
kushughulukia dhuluma na malalamiko ya ardhi na katika kipindi chote
tumejitahidi kupunguza malalamiko na yamepungua’’. Alisema Mbunge wa
jimbo la Isimani
‘’Ninaomba
mumpe ushirikiano, nimefanya naye kazi takriban miaka sita na
tumeelewana sana na nilimpa kazi nyingi kwa sababu ana uwezo, tofauti
yangu mimi na yeye ni kuwa, mimi ni mkali ila yeye ni mpole’’ alisema
Lukuvi
Kwa
mujibu wa Lukuvi, wakati wa uongozi wao, Wizara ya Ardhi ilipiga hatua
kubwa katika masuala mbalimbali yakiwemo mabadiliko ya mfumo wa utunzaji
kumbukumbu za ardhi sambamba na uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa.
Ameishukuru
Menejiment ya Wizara kwa kuonesha ushirikiano wakati wa kipindi chote
alichokuwa Wizara ya Ardhi na kuitaka menejiment hiyo kumpa ushirikiano
Waziri wa sasa Dkt Mabula.
Kwa
upande wake Dkt Mabula mbali na kumpongeza mhe Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumteua kuwa
Waziri wa Ardhi alimshukuru Lukuvi kwa kumpa uhuru wa kufanya kazi
wakati wote alipokuwa wakifanya kazi pamoja.
Alisema,
katika kipindi cha uongozi wao, wizara ya ardhi imefanya mambo mengi
kwa lengo la kuondoa changamoto za sekta ya ardhi na kubainisha kuwa
mafanikio yote yalitokana na ushirikiano na menejiment ya wizara.
‘’Mengi
yamefanyika kuondoa changamoto kwa ushirikiano na timu nzima ya
Menejiment, umenilea vizuri, malezi na imani uliyokuwa nayo ni wazi nina
deni kubwa la kulipa katika utendaji kazi’’
Waziri
Dkt Mabula aliongeza kuwa, pamoja na mambo mengine lakini msisitizo wa
wizara yake kwa sasa mbali na mambo mengine ni vipaumbele vya rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika masuala ya
uwekezaji na mifumo ya utunzaji kumbukumbu za ardhi.
Aliyekuwa
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa jimbo
la Isimani mkoani Iringa William Lukuvi aliondolewa nafasi ya uwaziri
katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mapema januari
mwaka huu. Lukuvi aliteuliwa kwa mara ya kwanza nafasi ya uwaziri mwaka
1995 katika iliyokuwa wizara ya kazi na baadaye kuhudumu Ofisi ya Waziri
Mkuu na baadaye Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambako
alidumu kwa miaka 8 tangu mwaka 2014.