SERIKALI YA SAMIA KUKAMILISHA MIRADI MINNE YA NHC ILIYOKWAMA DSM
Posted On: 14th February, 2022
Na Munir Shemweta, WANMMM
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amesema
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuendelea na ujenzi wa miradi ya
Shirika la Nyumba la Taifa iliyosimama.
Miradi
ya Shirika la Nyumba la Taifa iliyokwama Dar es Salaam ni ule wa Kawe
na Morocco Square na miradi hiyo ilisimama tangu mwaka 2017 kutokana na
changamoto mbalimbali zikiwemo za kifedha na mabadiliko ya baadhi ya
maboresho kwenye majengo ya Morocco Square.
Naibu
Waziri wa Ardhi alieleza hayo Bungeni tarehe 9 Februari 2022 wakati
akichangia hoja iliyowasilishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi,
Maliasili na Utalii.
“Serikali
iko tayari kukamilisha miradi iliyokuwa imesimama inayojengwa katika
Kiwanja No.300 Regent Estate, Kiwanja No. 711, na Moroco Square.”
Alisema Ridhiwani Kikwete.
Alisema,
serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha miradi ya NHC iliyokwama
inakamilika ili iweze kukaa vizuri na katika hatua ilizofanya Shirika la
Nyumba la Taifa ni kuomba kuchukua fedha kutoka vyanzo vyake vingine au
kukopa katika taasisi za fedha li kukamilisha miradi iliyokwama.
Hata
hivyo, Ridhiwani aliwaambia wabunge kuwa, chini ya Rais Samia Suluhu
Hassan Serikali ilielekeza kamati inayosimamia madeni iangalie vizuri
yale yaliyoombwa na NHC ambapo katika kuchakata kwake liliruhusiwa
Shirika kukopa shilingi bilioni 44.7 ili kukamilisha miradi hiyo.
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, kati ya fedha hizo shilingi bilioni 19
zinaenda plot 300 na kiasi kilichobaki kiende kwenye mradi wa Morocco
Square. Hata hivyo, kuhusu eneo la Kawe maelekezo ni kuwa Shirika likae
na Mwekezaji Mwenza Kampuni ya Al-Gurey-Dubai kuona namna bora ya
kuendelea na mradi wa eneo hilo.
Naibu
Waziri Ridhiwani alisema, baada ya mazungumzo na Mwekezaji Mwenza hatua
iliyofikiwa baada ya mikutano mitatu ni kwamba mbia anaenda kuwasiliana
na wenzake ili mambo watakayokubaliwa basi waje kuzungumza kwa pamoja.