MSAJILI MABARAZA AJA NA MIKAKATI YA KUPUNGUZA MASHAURI YA ARDHI NCHINI
Posted On: 28th January, 2022
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Katika
kuhakikisha mlundikano wa mashauri ya migogoro ya ardhi unapungua
nchini, Msajili wa Mabaraza ya Ardhi Stela Tullo ameelekeza Wenyeviti wa
Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwenda kusikiliza mashauri katika
wilaya nyingine ambazo hazina wenyeviti.
Akizungumza
katika maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma Stela
alisema, lengo ni kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati na haraka
sambamba na kusogeza huduma karibu na wananchi.
‘’Katika
kusogeza huduma karibu na wananchi tumeamua kusogezea huduma karibu
wananchi ambapo tumejiwekea mikakati na kuelekeza Wenyeviti wa Mabaraza
ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwenda wilaya nyingine ambazo hazina
wenyeviti kusikiliza mashauri ya wananchi na siyo wananchi kuwafuata
wenyeviti walipo’’. Alisema Stella
Kwa
mujibu wa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya nchini
Stella Tullo, kwa sasa kuna jumla ya Mabaraza 72 yanayotoa huduma na
kati hayo Mabaraza 28 hayana wenyeviti waliopangiwa vituo katika wilaya
hizo na kufanya wale wenyeviti wa wilaya za jirani kwenda kufanya kazi
huko.
‘’Hivi
sasa tuna jumla ya Mabaraza 72 na kati ya hayo 28 hayana wenyeviti
hivyo kuna ratiba tumewapangia wenyeviti kwenda kusikiliza mashauri
kwenye wilaya hizo jambo linalowapunguzia wananchi mzigo wa kusafiri
kutoka wilaya moja kwenda nyingine.
Maonesho
ya wiki ya sheria yalianza tarehe Januari 23, 2022 na kufunguliwa na
Rais wa Zainzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Husein Ally
Mwinyi na yanatarajia kufikia kilele siku ya jumamosi tarehe januari 29,
2022.